DIRA YA MAENDELEO 2025/2050 KUIMARISHA NA KUDUMISHA UHURU NA FURAHA KWA WATANZANIA.


Waziri wa nchi ofisi ya Rais- Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Alexander Mkumbo amesema lengo la Dira ijayo ya maendeleo ya mwaka 2025/2050 ni kuinua ustawi wa watanzania wote kama nyenzo mama ya kuimarisha na kudumisha uhuru na furaha kwa kila Mtanzania.

Leo Julai 27, 2024 wakati akihutubia mamia ya wananchi wa mikoa ya kanda ya kaskazini wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025/ 2050 Jijini Arusha, Prof. Kitila amesisitiza pia umuhimu wa kuweka mkazo na kuwekeza kwenye mageuzi mbalimbali ya kiuchumi, elimu, afya na miundombinu ili kufikia malengo tarajiwa.

" Tunapotafakari maudhui ya dira yetu ijayo ya mwaka 2025/2025, tuna vyanzo vikubwa vinne vya maarifa na taarifa ikiwemo kujifunza kutokana na uzoefu wetu wenyewe wa miaka 25 iliyopita na miaka zaidi ya 60 tangu nchi yetu ipate uhuru na kuundwa kwa jamhuri ya Muungano wa Tanzania" amesisitiza Waziri Kitila Mkumbo.

Prof. Mkumbo amesema kutokana na uzoefu huo ndipo Taifa litakapojua mambo gani yenye kustahili kupewa uzito katika kujipatia maendeleo lakini pia kama Taifa, linaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea kwa kasi na ambazo zina mazingira ya kufanana na nchi ya Tanzania.

Aidha Waziri Prof. Mkumbo amesema baad ya kukusanya maoni ya wananchi, kutaandaliwa rasimu ambayo baadae itarudishwa kwa wananchi ili kuiona na kutoa maoni yao kabla ya kuingizwa kwenye mchakato wa maamuzi ya kupitisha rasmi rasimu hiyo ili kuwa Dira mpya ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025/2050.

Post a Comment

Previous Post Next Post