Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kuwa ni faraja kuona maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwa shirikishi yanatekelezwa kwa makundi mbalimbali katika taifa.
Balozi Batilda ametoa kauli hiyo mapema siku ya Jumamosi tarehe 27 Julai 2024 akiwakilisha mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini wakati wa Kongamano la Pili la Kikanda Kuhusu Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025-2050 linalofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo.
Amesema kuwa kutokana na mchakato ulivyo, wao kama Kanda ya Kaskazini wamekuja na makundi mbalimbali kutoka sekta tofautitofauti nchini kama vile wafugaji, wakulima, wavuvi, wajasiriamali miongoni mwa makundi mengine ili waweze kutoa maoni yao ya namna wanataka Tanzania iwe kwa miaka 25 ijayo.
"Hakika tumeona ushirikishwaji mkubwa katika mikoa yetu, mmetembea katika mikoa yetu minne, mmeongea na viongozi lakini mmeongea na wananchi, mmoja mmoja kwa makundi, na hili tunalolifanya sasa ni mwendelezo wa kuhakikisha kwamba dira hii itakuwa bora zaidi kuliko iliyopita kwa maana ya ushirikishaji mkubwa ili kila Mtanzania aone kwamba yeye ni sehemu ya dira hii ya 2050" Ameeleza Dkt. Batilda.
Aidha amemshukruu Rais Samia kwa kuanzisha mchakato wa dira ya miaka 25 ijayo, na viongozi waliopita kwa kutekeleza dira inayomalizika ambayo imetekeleza miradi mbalimbali ya wananchi na kukuza ustawi wao katika kada tofautitofauti.
"Ninyi wote ni mashahidi wa jinsi gani dira yetu ya 2000/2025 ilivyoweza kuzaa matunda katika utekelezaji wake, matunda ambayo tumeyashuhudia katika kuboresha maisha ya wananchi, katika kuimarisha miundombinu na huduma mbalimbali, tumeona kupitia dira ile ta 2025 tumeweza kuongeza udadi ya shule, shule za kata zilianzishwa na tumeweza kuona uimarishwaji wa miundombinu barabara zikaongezeka" Ameeleza Dkt. Batilda.
Kongamano hili la kikanda linafanyika mkoani Arusha baada ya kukamilika mkoani Mwanza kwa mara ya kwanz. Baada ya kukamilika kwa ukanda huu wa kaskazini, litafanyika Jijini Mbeya ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyetaka wananchi washirikishwe kwenye uandishi wa dira hiyo ya maendeleo ya mwaka 2025/2050.