Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Doto Biteko amewataka washiriki wa kongamano la maandalizi ya dira ya Taifa 2050 kutafakari kuhusu ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini Tanzania, mahitaji tuliyonayo pamoja na rasilimali zilizopo ili kuoanisha mambo hayo kwenye mipango ya nchi.
Kufuatia hali hiyo Dkt. Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye Kongamano la kikanda la kukusanya maoni ya dira ya maendeleo ya 2050 leo Julai 20, 2024, amezisihi pia taasisi za serikali na sekta binafsi kujitokeza na kutoa maoni yao kutokana na uzoefu walionao katika kuhudumia jamii ya kitanzania.
"Maendeleo yanapotokea ndipo mahitaji pia yanapoongezeka. Changamoto kubwa tuliyonayo, mahitaji tuliyonayo na rasilimali tunazokusanya kupitia kodi na vyanzo vingine je vitatupa majibu ya tunachokitaka? lazima tujiulize sote. Wananchi tunaongezeka kila wakati maana yake mahitaji pia yanaongezeka." Amesema Dkt. Biteko
Biteko amesema ikiwa tutafahamu vyema kuhusu mahitaji yanayoongezeka kila siku kutokana na idadi ya watu pamoja na ufinyu wa rasilimali zilizopo nchini, itasaidia kupata majibu ya Tanzania inayotakiwa na watanzania miaka 25 baadae.