Afisa Tarafa wa Tarafa ya Katerero iliyoko wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Ndugu Bwanku M Bwanku Jana Jumamosi Julai 13, 2024 amefanya Kikao na Waganga wa Jadi au Waganga wa Tiba asili waliopo katika Tarafa ya Katerero wa Kata 3 ambapo ajenda kubwa ilikua kuwasisitiza Waganga hao kujiepusha na vitendo vya ukatili wa watu wenye ualbino, ramli chonganishi na kushirikiana na serikali kulinda amani na usalama wa Tarafa huku wakiendelea kutoa huduma zao kwa kufuata sheria na taratibu.
Kikao hicho na Waganga wa Jadi kimefanyika katika ofisi ya Mtendaji Kata Kemondo na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Kagera Ndugu Hermes Nyarubamba, Watendaji wa Kata ya Kemondo Ndugu Cyriacus Sosthenes, wa Kata ya Katerero Madam Sophia Busunge, wa Kata ya Bujugo Anna Barongo pamoja na Polisi Kata mbalimbali ambapo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima amepongeza hatua hiyo baada ya kupigiwa simu na Afisa Tarafa Bwanku kuwasalimia Wajumbe wakati kikao hicho na Waganga kikiendelea.
Kwenye Kikao hicho, upande wa Serikali na Waganga hao wamekubaliana kuhakikisha Waganga wote ambao hawana vibali wafuatilie kupata vibali vya kutoa tiba asili, kutoa taarifa ya Waganga wanaofanya ramli chonganishi, watakaojihusisha na vitendo vya ukatili wa albino ama jinsia pamoja na vitendo vyote vya utabibu ambavyo havikubaliki.