TARURA YAWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WAPYA 60 KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetoa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 60 wakiwemo Wahandisi, Mafundi Sanifu, Madereva, Watunza Kumbukumbu, Maafisa Ununuzi, Maafisa Mazingira na Waandishi Waendesha Ofisi ikiwa ni hatua muhimu ya kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na ufanisi katika kuhudumia wananchi.

‎Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika katika ukumbi wa Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma yamelenga kuwajengea uelewa watumishi hao kuhusu sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma pamoja na maadili yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

‎Akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TARURA, Bi. Azimina Mbilinyi amesema kuwa mafunzo hayo ni msingi muhimu wa kuwajengea uwezo watumishi wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uwazi na uzingatiaji wa maadili ya kazi.

‎Bi. Azimina amewataka watumishi hao kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo hayo kwa vitendo, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

‎Amesisitiza umuhimu wa kuwa na nidhamu, uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya TARURA akieleza kuwa utendaji wa kila mtumishi una mchango katika kufanikisha malengo ya Wakala.

‎"Kila mmoja wenu ana nafasi muhimu katika kufanikisha majukumu na malengo ya TARURA tumieni maarifa mliyopata zingatieni maadili na taratibu za utumishi wa umma na zaidi hakikisheni mwananchi anapata huduma bora na kwa wakati",  amesema Bi. Azimina.

‎Mafunzo hayo yametolewa na Wataalam kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) na katika mafunzo hayo watumishi wamepatiwa mada mbalimbali zinazohusu sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Post a Comment

Previous Post Next Post