TANZANIA YAKABIDHI TANI 52 ZA DAWA NA VIFAA TIBA DRC KUKABILIANA NA EBOLA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa takribani tani 52 za bidhaa za afya zenye thamani ya Shilingi milioni 220 kwa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo.

Akizungumza leo Septemba 5, 2026 jijini Kinshasa wakati wa makabidhiano ya msaada huo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania imefika DRC kutimiza ahadi iliyotolewa na Serikali ya Tanzania ya kuwasilisha msaada huo mara Serikali ya DRC ilipokuwa tayari kuupokea.

Dkt. Samizi amesema msaada huo unajumuisha vifaa vya kinga binafsi kwa wahudumu wa afya, vifaa tiba pamoja na bidhaa nyingine muhimu zinazohitajika katika mwitikio dhidi ya Ebola, zikiwa na lengo la kuwalinda wahudumu wa afya, kuimarisha huduma kwa wagonjwa na kusaidia kukata mnyororo wa maambukizi.

Amesema msaada huo uliahidiwa Agosti 19, 2026 wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Afya wa Ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo Waziri wa Afya wa Tanzania, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikabidhi kwa mfano sehemu ya msaada huo na kuahidi kuufikisha DRC katika eneo ambalo Serikali ya nchi hiyo ingependa kuupokea.

“Msaada huu ni ishara ya urafiki na undugu wa muda mrefu kati ya Tanzania na DRC. Virusi havitambui mipaka, na mshikamano wetu pia haupaswi kutambua mipaka,” amesema Dkt. Samizi.

Amesema Tanzania inaamini kuwa katika afya ya umma hakuna “mlipuko wao” na “usalama wetu”, bali kuna usalama wa afya wa pamoja, hivyo nchi zinapaswa kushirikiana kwa vitendo katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

Kwa upande mwingine, Dkt. Samizi ameupongeza uongozi wa Serikali ya DRC chini ya Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo kwa juhudi zinazofanyika katika kukabiliana na mlipuko huo, huku akiwapongeza wahudumu wa afya, jamii zilizoathirika na timu za mwitikio kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuokoa maisha na kukatiza maambukizi.

Amesema Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana na DRC, Umoja wa Afrika, Africa CDC, WHO pamoja na washirika wengine katika kuimarisha utayari, ufuatiliaji na mwitikio wa haraka dhidi ya milipuko ya magonjwa.

Katika kuwezesha upatikanaji na maandalizi ya msaada huo, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imehusika katika kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana na kuandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Serikali ya DRC.

Kwa upande wake, Dkt. Romain Muboyayi, Mkurugenzi wa Ofisi ya Waziri wa Afya, ambaye alipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali ya DRC, ameishukuru kwa dhati Serikali ya Tanzania na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msaada huo, akisema Tanzania na DRC ni nchi ndugu na majirani, hivyo hatua hiyo inathibitisha undugu, mshikamano na uhusiano wa karibu uliopo kati ya mataifa hayo.

Dkt. Muboyayi amesema msaada huo umewasilishwa wakati muhimu kwa DRC na utasaidia katika juhudi za Serikali ya nchi hiyo za kukabiliana na Ebola, akisisitiza kuwa ushirikiano na mshikamano wa nchi jirani ni muhimu katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa ambayo haina mipaka

Akikabidhi rasmi msaada huo kwa Serikali ya DRC, Dkt. Samizi amesema Tanzania itaendelea kuwa pamoja na DRC katika mapambano dhidi ya Ebola na dharura nyingine za afya ya umma, huku akisisitiza kuwa mshikamano wa Tanzania hautaishia katika tukio hilo bali utaendelea kwa vitendo kadiri ya uwezo wa Serikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post