Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) leo Septemba 5, 2026 imefanya ziara katika Manispaa ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam, kwa lengo la kutathmini namna wawekezaji wa shughuli za Bandari Kavu (ICD) wanavyoshirikiana na Halmashauri katika kuboresha miundombinu, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Kamati hiyo kukagua na kutembelea maeneo mbalimbali ya Bandari Kavu katika Manispaa ya Temeke, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Frolent Kyombo, amesema ziara hiyo imelenga kuona namna shughuli za Bandari Kavu zinavyoweza kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara inayotumika katika usafirishaji wa makasha ya mizigo.
Mhe. Kyombo amesema ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka, huku uwepo wa Bandari Kavu ukisaidia kupunguza msongamano wa makasha katika eneo la bandari kwa kuyahamisha na kuyaelekeza katika maeneo mbalimbali, hali iliyoongeza urahisi wa upokeaji na usafirishaji wa mizigo na kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuhakikisha barabara zinazotumika katika shughuli hizo zinaendelea kuwa imara na zenye ufanisi.
Aidha, amesema Kamati imeangalia namna Manispaa ya Temeke inavyoweza kunufaika zaidi na shughuli za Bandari Kavu kupitia ukusanyaji wa mapato kwa kushirikiana na wawekezaji na wadau wanaoendesha shughuli hizo.
Kwa mujibu wa Mhe. Kyombo, mapato yatakayopatikana yanaweza kutumika kuwekeza katika huduma na miundombinu muhimu ya wananchi, ikiwemo afya, elimu na barabara, huku mazingira bora ya biashara yakiendelea kuwekwa kwa wawekezaji.
Mhe. Kyombo amesema Kamati itaendelea na majadiliano pamoja na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa ya Temeke ili kubaini maeneo ya ushirikiano kati ya Halmashauri na wadau wa Bandari Kavu, lengo likiwa ni kuhakikisha Halmashauri inanufaika na shughuli hizo kupitia mapato, wakati wawekezaji nao wanaendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuchangia katika maendeleo ya Manispaa ya Temeke.
