Afisa Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Kagera Ndugu Bwanku M Bwanku Juzi Jumanne Juni 30, 2026 amekua mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika Kata ya Rubale na kuhudhuriwa na watoto wenyewe, wananchi, viongozi na watumishi mbalimbali wa Serikali.
Kwenye hotuba yake kama mgeni rasmi, Bwanku amesisitiza umuhimu wa familia na jamii kumlinda mtoto kwa kuhakikisha anapata elimu, malezi bora, kumlinda na ukatili ili kujenga Taifa imara la baadae chini ya kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu yaliyounganishwa na Siku ya Familia isemayo MTOTO NI MALEZI, MSINGI WA FAMILIA BORA KWA TAIFA IMARA.
Aidha, Afisa Tarafa Bwanku aliwasisitiza watoto kutoogopa kuripoti vitendo vya ubakaji, ulawiti, unyanyasaji na aina yoyote ya ukatili pindi wakifanyiwa ili Serikali ichukue hatua stahiki za kumlinda mtoto.
"Niombe sana familia na jamii kumlinda mtoto kwa gharama yoyote ili kuwa na Taifa imara leo na kesho. Pia watoto someni kwa bidii zote kwani tayali Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeondoa ada mashuleni na kuboresha miundombinu ya elimu kuanzia Shule za Msingi hadi Sekondari ili msome vyema" Alisisitiza Bwanku akizungumza kwenye Maadhimisho hayo.
Maadhimisho haya kwa ngazi ya Kata yaliratibiwa na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Bukoba kwa kushirikiana na World Vision ambapo kwa kipindi cha wiki moja kabla ya maadhimisho elimu juu ya kupinga ukatili wa Watoto, ulinzi na usalama wa Mtoto na stadi za kazi imetolewa kwa Watoto kwenye shule mbalimbali za Msingi na Sekondari.
