Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameitaka Menejimenti ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuchukua hatua za kuboresha ustawi wa mabaharia nchini ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa ajira melini, kuanzisha kanzidata (database) ya mabaharia wote wa Tanzania na kuimarisha taasisi inayosimamia maslahi yao
Akizungumza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwanga Community Centre mkoani Kigoma leo tarehe 25 Juni, 2026 Prof. Mbarawa amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi, mafunzo na usalama wa mabaharia ili kuongeza ushindani wao katika soko la ajira la kimataifa
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa maadhimisho hayo kwa niaba ya katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa usafiri na Mazingira, Bi.Stella Katondo amesema maadhimisho ya mwaka 2026 yamehusisha shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji elimu ya usalama majini, maonesho ya wadau, kampeni za uhamasishaji utunzaji mazingira ya maji pamoja na mazoezi ya vitendo ya uokozi yaliyofanyika katika ziwa Tanganyika ambapo shughuli hizo zimefanikisha kuongeza uelewa wa wananchi na wadau kuhusu mchango wa mabaharia katika maendeleo ya uchumi na biashara
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema Serikali kupitia TASAC imeendelea kuimarisha usalama wa usafiri majini, kusimamia utekelezaji wa viwango vya kimataifa na kuboresha mazingira ya mabaharia ili kuongeza fursa za ajira ndani na nje ya nchi
Awali akitoa salamu ya mkoa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Rashid Chuachua alisema maadhimisho hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kutokana na elimu iliyotolewa kuhusu usalama majini na fursa zilizopo katika uchumi wa buluu na kueleza kuwa Mkoa wa Kigoma utaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuendeleza shughuli za usafiri na biashara kupitia Ziwa Tanganyika
Maadhimisho ya mwaka huu yaliyoanza tarehe 22 Juni, 2026 yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora katika Sekta ya Usafiri Majini” na kuhusisha wadau wa kisekta.
