TASHICO KUKAMILISHA UKARABATI WA MELI YA MV LIEMBA MWISHONI MWA JULAI


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inatarajia kukamilisha ukarabati wa meli ya MV Liemba mwishoni mwa Julai 2026, hatua itakayorejesha huduma muhimu za usafiri na usafirishaji katika Ziwa Tanganyika

Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Kigoma baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa meli hiyo, ambapo alibainisha kuwa mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 33 umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na kueleza kuwa kazi zilizobaki ni pamoja na kuipandisha meli kwenye chelezo kwa ajili ya ukaguzi wa sehemu za chini ya maji pamoja na kutoa na kufunga upya shafti ya meli

Aidha, alisema kuwa majaribio ya meli yanatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Julai ili kubaini na kurekebisha changamoto zozote zinazoweza kujitokeza kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma

“Tunatambua umuhimu wa MV Liemba kwa wananchi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa pamoja na wadau wengine wa usafiri katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika  Serikali imejipanga kuhakikisha meli hii inaanza kufanya kazi rasmi kabla ya mwisho wa mwezi Julai mwaka huu,” alisema Prof. Mbarawa

Aliongeza kuwa kukamilika kwa ukarabati huo kutaimarisha usalama wa usafiri majini kutokana na maboresho yaliyofanyika katika mifumo ya umeme, mawasiliano na vifaa vingine muhimu vya uendeshaji wa meli

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Ukarabati wa MV Liemba, Mhandisi Ernest John, alisema kuwa kazi za ukarabati zinaendelea vizuri na zinazingatia viwango vya kitaalamu, huku majaribio ya awali ya meli yakitarajiwa kufanyika Julai 17 na 18, 2026.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutarejesha uwezo wa MV Liemba kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wanaotegemea usafiri wa majini katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika

Post a Comment

Previous Post Next Post