Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania ( TASAC) iliyochini ya Wizara ya Uchukuzi imepeleka boti ya kisasa ya uokoaji Mkoani Kigoma kwa lengo la kuimarisha usalama wa usafiri majini na kuwalinda wavuvi pamoja na wananchi wanaotumia Ziwa Tanganyika katika shughuli zao za kila siku
Akizungumza mkoani Kigoma tarehe 25 Juni 2026, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo ya usalama majini kwa kuhakikisha vyombo vya kisasa vya uokoaji vinapatikana kwenye maziwa makuu nchini
Prof. Mbarawa alisema boti hiyo ina uwezo wa kukimbia kwa kasi ya noti 45 kwa saa, sawa na takribani kilomita 75 kwa saa, jambo litakalowezesha kufikika haraka katika maeneo ya matukio ya dharura na kuokoa maisha ya watu
“Wavuvi na wadau wote wanaotumia Ziwa Tanganyika sasa watakuwa salama zaidi kutokana na uwepo wa boti hii ya kisasa ya uokoaji ,Serikali imewekeza shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya ununuzi wa boti za uokoaji ambazo zitasaidia kuimarisha huduma za uokoaji na usalama majini,” alisema Prof. Mbarawa
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutambua umuhimu wa kuimarisha usalama wa Watanzania wanaofanya shughuli zao katika maziwa mbalimbali nchini
“Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usalama katika maziwa yetu, tunatambua kuwa usalama wa shughuli za majini unachangia kukuza uchumi na kuongeza kipato kwa wananchi wanaotegemea rasilimali za maji katika kujipatia riziki” aliongeza
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema shirika hilo limepeleka boti maalumu ya uokoaji Mkoani Kigoma itakayosaidia kuimarisha usalama wa usafiri majini na kulinda maisha ya wavuvi pamoja na watumiaji wengine wa Ziwa Tanganyika
Alieleza kuwa kutokana na changamoto za ajali za majini zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzama kwa vyombo vya usafiri, boti hiyo itaongeza uwezo wa kutoa huduma za haraka za uokoaji na kuokoa maisha ya wananchi.
