UJENZI GATI LA ABIRIA KIGOMA KUKAMILIKA SEPTEMBA 2027


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa  Gati jipya la kuhudumia abiria kwenye Bandari ya Kigoma unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2027, huku mradi huo wa kimkakati ukigharimu shilingi bilioni 32.5.

Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Kigoma baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati hiyo, ambapo alieleza kuwa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 23.5 na kazi zinaendelea kwa kasi kulingana na ratiba iliyopangwa

Alibainisha kuwa mara baada ya kukamilika, bandari hiyo itakuwa na gati lenye urefu wa mita 130 na upana wa mita 30, uwezo ambao utaruhusu meli kubwa kutia nanga na kuhudumia abiria kwa ufanisi zaidi na kuongeza kuwa mradi huo utahusisha pia ujenzi wa yadi, maeneo ya maegesho ya magari pamoja na barabara za maingiliano

“Bandari hii itakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa biashara na uchumi katika Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Maziwa Makuu kwa ujumla kwa kuwa itawezesha kupokea meli kutoka nchi jirani ikiwemo Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hivyo kuongeza fursa za biashara, usafirishaji na uwekezaji” alisema Prof. Mbarawa

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya usafiri na usafirishaji mkoani Kigoma, ikiwemo ujenzi wa gati la mizigo, maendeleo ya reli ya kisasa (SGR) pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara inayounganisha reli, bandari na maeneo ya uzalishaji

Prof. Mbarawa aliipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa usimamizi wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zake

Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo Mha. Peter Macharja alisema utekelezaji unaendelea vizuri na kwamba kuchelewa kuanza kwa baadhi ya shughuli za awali hakutaathiri lengo la kukamilisha mradi huo ifikapo Septemba 2027, ambapo bandari hiyo itaanza kutoa huduma kwa kiwango cha kisasa na kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika.

Post a Comment

Previous Post Next Post