BANDARI YA KIGOMA KUHUDUMIA TANI MILIONI MOJA ZA MIZIGO KWA MWAKA IKIKAMILIKA


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Bandari ya Kigoma inayoendelea kuboreshwa itakuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni moja za mizigo kwa mwaka mara baada ya kukamilika, hatua inayotarajiwa kuimarisha biashara na usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)

Prof. Mbarawa amesema hayo Juni 25, 2026 mkoani Kigoma baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya maboresho ya bandari hiyo, ambapo alieleza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa mradi huo ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika

Alisema kuwa kwa sasa kiwango kikubwa cha mizigo kinachosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda DRC kinaonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari za ndani ya nchi ili kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa kibiashara katika ukanda huo.

Prof. Mbarawa alibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi umeendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya usafiri, akitolea mfano mafanikio yaliyopatikana katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na uwekezaji unaoendelea katika Bandari ya Kigoma

Aidha, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu, huku ukienda sambamba na uwekezaji wa meli mpya za kisasa zitakazoongeza uwezo wa kusafirisha mizigo katika Ziwa Tanganyika

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPA  Dkt. Baraka Mdima amesema tayari mkandarasi amekabidhiwa eneo la ujenzi na kazi zinaendelea kwa lengo la kuhakikisha bandari hiyo inakuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji wa mizigo kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Post a Comment

Previous Post Next Post