Katika hatua muhimu ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kukuza uwekezaji wa viwanda kati ya Tanzania na Indonesia, Kampuni ya Tanganyika Fats Allied Products and Foods Ltd ya Kigoma, Tanzania, imesaini Makubaliano ya Awali ya Ushirikiano (MOU) na Kampuni ya Indo Sultan Jaya Group ya Jakarta, Indonesia, kwa ajili ya uwekezaji wa pamoja wa kuanzisha kiwanda cha kisasa cha sabuni na bidhaa za chakula nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, na kupanua fursa za ajira kupitia uwekezaji wa teknolojia na ununuzi wa mitambo na mashine kutoka Indonesia.
Tukio hilo limehusisha ushirikiano wa ngazi ya G2G (Government to Government), B2B (Business to Business), ICCI na TNCC, likionesha nguvu ya diplomasia ya kiuchumi katika kuunganisha sekta binafsi na serikali za nchi hizo mbili.
Akizungumzia makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC), Bw. Abdul Mwilima, amesema,
“Hii ni hatua kubwa sana kwa sekta binafsi ya Tanzania. Ushirikiano huu unaonesha matokeo ya diplomasia ya kiuchumi inayoendelea kuzaa matunda, na Tanzania inaendelea kuwa kivutio cha uwekezaji wa viwanda.”
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mheshimiwa Suleyman Saleh, amesema,
“Makubaliano haya ni ushahidi wa mahusiano imara kati ya Tanzania na Indonesia. Tutahakikisha mazingira ya biashara yanaendelea kuwezeshwa ili miradi kama hii itekelezwe kwa ufanisi na manufaa ya pande zote.”
Mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya viwanda, uhamishaji wa teknolojia, na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani nchini Tanzania, hususan katika sekta ya sabuni na bidhaa za chakula.
Vilevile, makubaliano haya ni mwendelezo wa utekelezaji wa MOU ya awali iliyosainiwa kati ya ICCI na TCCIA/TNCC chini ya uongozi wa Rais Vicent Minja jijini Jakarta, Indonesia, Februari 2024, ambayo ililenga kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Uwekezaji huu unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya viwanda na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uzalishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
