TRENI YA SGR IMERAHISISHA WANANCHI KUFIKA HARAKA KWENYE MAJUKUMU YAO - PACHO


Dereva wa treni ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), Joseph Pacho, amesema huduma ya reli hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafiri wa wananchi kwa kuwafikisha kwa haraka kwenye shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya #NusuMudaKoteKote iliyoandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya reli ya kisasa ya SGR pamoja na kuadhimisha miaka miwili tangu kuanza kwa huduma hiyo nchini.

Kampeni hiyo inalenga kuonyesha mafanikio ya reli ya SGR katika kupunguza muda wa safari, kuboresha huduma za usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli za wananchi kupitia usafiri wa kisasa wenye kasi na usalama. 

Pacho amesema, treni ya SGR imeendelea kuwa chaguo la wengi kutokana na kasi, utulivu na mazingira mazuri ya safari.

Amesema tangu aanze kazi ya kuendesha treni za abiria za SGR, ameshuhudia namna huduma hiyo ilivyosaidia wananchi kuokoa muda na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Treni hii ya umeme ina kasi. Unaweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa muda mfupi zaidi,” alisema.

Joseph amesema tofauti na baadhi ya mifumo mingine ya usafiri, treni ya SGR imejengwa katika mazingira yanayowapa abiria faraja wakati wa safari kutokana na utulivu wake.

“Pia iko comfortable zaidi, hakuna kelele,” alisema.

Ameongeza kuwa anajivunia kuwa sehemu ya watendaji wanaohakikisha wananchi wanapata huduma bora ya usafiri inayowawezesha kufika salama na kwa wakati katika maeneo yao mbalimbali.

“Tangu kuanza kwa majukumu yetu ya kubeba abiria, najivunia kazi hiyo kwa sababu tunasaidia wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili waweze kutimiza majukumu yao ya kiuchumi na kijamii,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post