KINACHONIVUTIA KATIKA USAFIRI WA SGR NI KUFIKA MAPEMA KULE NAPOKWENDA - ABIRIA


Baadhi ya abiria wanaotumia huduma ya usafiri wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) wameendelea kueleza kuridhishwa kwao na huduma hiyo kutokana na kasi, ubora na faraja inayopatikana wakati wa safari.

Miongoni mwao ni Fatma Twaha, ambaye amesema moja ya mambo yanayomvutia zaidi katika usafiri wa SGR ni uwezo wa kufika mapema katika maeneo anayokwenda bila kuchoka.

Amezungumza Mei 08, 2026 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya #NusuMudaKoteKote yenye lengo la kuadhimisha miaka miwili tangu kuanza kwa huduma ya SGR pamoja na kuhamasisha matumizi ya reli hiyo ya kisasa inayorahisisha usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli za wananchi. 

Fatma amesema safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kupitia SGR imekuwa rahisi na ya haraka zaidi kutokana na muda mfupi unaotumika kufika.

“Kinachonivutia katika usafiri wa SGR ni kufika mapema. Saa moja na dakika 40 unakuwa umeshafika na hauchoki,” alisema.

Amesema tofauti na usafiri wa barabara unaokumbwa na changamoto za foleni, huduma ya SGR imekuwa msaada mkubwa kwa watu wenye shughuli mbalimbali kutokana na kuokoa muda na kuwafanya abiria kusafiri kwa utulivu.

“Uwe unakwenda harusini au kwenye shughuli zako nyingine, hauchoki. Kwa gari unachoka ukilinganisha na foleni za mji huu,” alisema.

Fatma pia ameeleza kufurahishwa kwake na ubora wa huduma zinazotolewa ndani na nje ya treni, akisema mazingira ya usafiri huo yanaendana na viwango vya kisasa.

“Huduma zote za ndani ya treni na nje zinavutia. Kwa kifupi huduma zote za SGR zinavutia,” alisema.

Aidha amewahamasisha Watanzania wengi zaidi kutumia usafiri wa SGR kutokana na urahisi, kasi na gharama zake ambazo amesema zinaendana na huduma zinazotolewa.

Post a Comment

Previous Post Next Post