Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Mbunge mstaafu wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba, ametoa wito kwa Viongozi wa dini kuongeza dua, kwa Nchi, Viongozi na kwake yeye mwenyewe.
Akihutubia mkusanyiko huo mkubwa wa viongozi wa dini na wananchi, Makamba amewataka Masheikh na walimu wa dini kuendelea kuiombea nchi dua ili wale waliopewa dhamana ya kutoa hukumu waweze kutekeleza wajibu huo kwa uadilifu.
“Wazee wangu, masheikh wangu, walimu wangu, ombi langu mimi kwenu ni dua, dua kwangu mimi binafsi lakini dua kwa nchi yetu, dua kwa viongozi wetu, na dua kwa watu wote wenye mamlaka ya kuhukumu, wahukumu kwa haki, kwa hekima na kwa busara ili jamii yetu iendelee kuwa ya umoja, mshikamano, upendo, amani, usalama na utulivu ili tuirithishe kwa watoto wetu ikiwa hivyo”, ameeleza Makamba.
Makamba ameeleza kufarijika kwake na wingi wa watu waliojitokeza, akisema mahudhurio hayo ni kielelezo cha utamaduni wa watu wa Tanga wa kupendana na kushirikiana katika mambo ya heri. Ameahidi kuendeleza utamaduni huo wa kufuturisha mradi Mwenyezi Mungu akimjalia uzima na riziki.
