MBUNGE WA JIMBO LA KIBAMBA ASEMA HATOBAGUA DINI WALA KABILA


Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema ataendelea kuwatumikia wananchi wote wa jimbo hilo bila kubagua dini, kabila wala makundi ya kijamii.

Mbunge Kairuki ameyasema hayo wakati wa futari aliyoiandaa na kuwakutanisha makundi mbalimbali ya jamii katika Jimbo la Kibamba. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa Serikali, viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Aidha, watu wenye ulemavu pia walihudhuria futari hiyo ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii katika shughuli za kijamii na maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge Kairuki alisisitiza kuwa uongozi wake unalenga kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa usawa bila kuangalia tofauti za kidini, kikabila au hali zao za kijamii.

Alieleza kuwa futari hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuimarisha upendo, mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi wa Jimbo la Kibamba pamoja na kuendeleza utamaduni wa kushirikiana katika mambo ya kijamii.

Mbunge huyo pia aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na ushirikiano ili kuendelea kujenga maendeleo ya Jimbo la Kibamba na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post