EMWANI CAFE YAUNGA MKONO MRADI WA YANGA SOCCER SCHOOL KUKUZA VIPAJI VYA VIJANA


Jitihada za Yanga SC katika kuendeleza soka la vijana zimepata msukumo mpya baada ya EMWANI Cafe kutangaza kuwekeza katika mradi wa Yanga Soccer School, hatua inayotajwa kuongeza fursa kwa vijana wenye vipaji nchini.

Ushirikiano huo unakuja wakati wadau wa michezo wakiongeza nguvu katika kusaidia programu za maendeleo ya vijana, sambamba na maono ya kocha mashuhuri Pitso Mosimane ambaye amekuwa akihimiza uwekezaji wa muda mrefu katika soka la vijana barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano Machi 25, 2025 Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Alikamwe, amesema kuwa kupitia ushirikiano huo, mashindano maalum yameandaliwa na yatafanyika Machi 28, 2026 katika kituo cha TFF Kigamboni, yakilenga kutoa jukwaa la kusaka vipaji vipya.

Kwa upande wake, Mmiliki wa EMWANI Cafe, Leo Mendez, amesema kampuni yake imeamua kuwekeza katika mradi huo kama sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya michezo na kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

“Kama mdau wa michezo na mfanyabiashara, ninaamini katika kuwapa vijana mazingira ya kukua. Ushirikiano huu na Yanga ni njia ya kuchangia mustakabali wa soka la Tanzania,” alisema.

Emwani Coffee Ltd (EMWANI CAFE)* ni kampuni ya kahawa ya Kitanzania iliyoanzishwa mwaka 2025, ikiwa na makazi yake jijini Dar es Salaam na kujikita katika uzalishaji, uchakataji na uuzaji wa kahawa ya ubora wa juu, huku ikilenga kuonesha utambulisho na urithi wa kahawa ya Afrika Mashariki katika soko la ndani na la kimataifa. 

EMWANI COFFEE LTD ni Kampuni inaendeshwa kupitia mifumo miwili mikuu, upande wa Emwani Coffee Roasters, unaoshughulika na kuchakata, kufungasha na kuuza kahawa, na upande wa Emwani Café, unaolenga kutoa huduma ya vinywaji pamoja na kuwa kituo cha kukuza utamaduni wa kahawa huku dira yake ni kufanya kahawa ya Tanzania itambulike duniani si tu kwa ladha, bali pia kwa hadithi, asili na watu wanaoizalisha

Post a Comment

Previous Post Next Post