MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI AFRIKA MASHARIKI KUENDELEA KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA NA UCHUMI


Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, yuko nchini Tanzania kwa ziara rasmi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ili kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa upande wa Tanzania, akiongozana na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mhe. Ndejembi amesema mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unaendelea kutoa manufaa makubwa hususan katika utoaji wa ajira, ambapo jumla ya ajira 12,000 zimetolewa kwa vijana na wananchi wa Tanzania na Uganda wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 79 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2026. Ameeleza kuwa pindi utakapokamilika, mradi huo utakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 246,000 ya mafuta ghafi kwa siku, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato kwa nchi za Tanzania na Uganda.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira na nia yake ya dhati katika utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati, akisema umeleta mafanikio makubwa na mapinduzi ya kiuchumi kwa nchi za Afrika Mashariki.

Dkt. Nankabirwa amesema kuna umuhimu wa kuwa na utaratibu maalumu wa kuwatambua wafanyakazi wanaopata ajira katika miradi mikubwa ya kimkakati kama EACOP, ili waweze kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mingine ijayo kulingana na uzoefu, uadilifu na uwezo wao kazini. Ameitaja miradi ya gesi na umeme kuwa miongoni mwa miradi itakayofaidika na rasilimali watu waliopata uzoefu kupitia EACOP.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga una urefu wa kilomita 1,443, ambapo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1,147 zipo nchini Tanzania. Kwa upande wa Tanzania, mradi huo utakuwa na vituo vinne vya kusukuma mafuta, huku Uganda ikiwa na vituo viwili, na kufanya jumla ya vituo vya kusukuma mafuta kuwa sita.

Post a Comment

Previous Post Next Post