DKT. MWIGULU AIAGIZA TRC KUENDELEA KUZINGATIA USALAMA WA SAFARI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutanguliza usalama wa wananchi kwa kutoa taarifa mapema pale panapobainika uwezekano wa hatari, badala ya kuendelea na safari za reli kwa presha au mihemko inayoweza kusababisha madhara.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo Januari 02, 2025, wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Kidete mkoani Morogoro, akiwa katika ziara ya kukagua athari za mvua kubwa zilizosababisha uharibifu wa miundombinu, ikiwemo daraja la reli katika eneo hilo.

Amesema kuwa Serikali imejipatia taarifa za awali zinazoonesha kuwepo kwa uharibifu katika eneo la daraja hilo, ambapo tuta la mto limeendelea kudhoofishwa na maji, hali iliyosababisha hatari kwa usalama wa miundombinu ya reli licha ya nguzo na muundo wa reli kuonekana bado imara.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, karibu nusu ya eneo la daraja hilo limeporomoka kwa umbali wa takribani mita 30 katika sehemu yenye nguzo zilizopo ndani ya mto, jambo linalohitaji tathmini ya kina ya kiusalama kabla ya kuendelea na safari.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Mwigulu amewataka wataalamu wa TRC kutokuwa na kigugumizi wala hofu katika kutoa tahadhari kwa wananchi pale wanapoona dalili za hatari, akisisitiza kuwa hatua za kuahirisha safari ni za kawaida na zinalenga kulinda maisha ya watu.

Ameeleza kuwa duniani kote, vyombo vya usafiri kama reli, ndege na meli hupewa kipaumbele cha usalama, ambapo safari husitishwa au kuahirishwa endapo hali ya hewa au mazingira yanaashiria uwezekano wa madhara.

Dkt. Mwigulu ametoa mfano wa baadhi ya reli za kisasa barani Ulaya ambazo zimesitisha safari kwa muda kutokana na mvua kubwa na upepo mkali unaoweza kuathiri mifumo ya umeme, akiongeza kuwa hata katika maeneo yenye theluji nyingi, safari za ndege huahirishwa kwa sababu za kiusalama.

Amesisitiza kuwa hakuna shinikizo lolote linalopaswa kuwalazimisha wahusika kuendesha safari endapo usalama haujaridhisha, akibainisha kuwa maisha ya Watanzania ni ya thamani kubwa kuliko ratiba za usafiri.

Amehitimisha kwa kuagiza TRC na taasisi husika kuchukua hatua za haraka kurekebisha uharibifu wa tuta na kingo za mto, pamoja na kufanya tathmini ya kitaalamu ya usalama, kabla ya kurejesha safari za reli katika eneo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post