Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Mhe. Nadir Abdullatif Al-wardy wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika usimamizi wa sekta ya maji nchini ikiwemo katika matumizi ya teknolojia mpya za usimamizi na uratibu wa maji nchini.
Mhe. Aweso amebainisha hayo leo Jumapili Januari 18, 2026 alipokutana na kuzungumza na Waziri Al-wardy jijini Dar Es Salaam wakati wa majumuisho ya pamoja yaliyowakutanisha Viongozi wa sekta ya maji kutoka Tanzania bara na Zanzibar baada ya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maji.
"Huu ushirikiano tuliouanzisha tutauendeleza na lazima tukubali kubadilika, teknolojia itumike kuleta mageuzi kwenye sekta ya maji ikiwemo pre Paid Meter ambayo tumeshaanza kuitekeleza ili kuondoa ubambikiaji wa bili na kuleta nidhamu katika matumizi ya maji.Ni lazima tukubali kutumia teknojia kuleta mageuzi kwenye sekta ya maji nchini."amesisitiza Waziri Aweso.
Kulingana na Waziri huyo, utekelezaji wa ufungaji wa mita hizo za malipo kabla ya matumizi umeshaanza, ukienda sambamba na matumizi ya teknolojia za utibuji wa maji yenye chumvi kutokana na kubainika uwepo wa maeneo mengi yenye changamoto ya chumvi nyingi kwenye maji yanayochimbwa ardhini.
Kwa upande wake Waziri Al-wardy amempongeza Waziri Aweso kwa kuendelea kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kusema Zanzibar wanaridhishwa na uongozi na jitihada zake katika kuimarisha sekta ya maji nchini na kuahidi kuendelea kujifunza kutoka kwa Waziri Aweso katika kuboresha sekta ya maji Zanzibar.
