Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa Utumishi walio katika Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake kuacha tabia ya uonevu na matumizi ya lugha mbaya wanapowahudumia watumishi au wananchi wanaohitaji ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa Maafisa Utumishi, wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Menejimenti za Halmashauri za mkoa huo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
“Maafisa Utumishi msiwe Maafisa utu nusu, mtumishi au mwananchi anapokuwa na shida anapaswa kukuona Afisa Utumishi kwani wewe ndio unajua masuala ya kiutumishi, hivyo usitumie lugha mbaya wala kumuonea mtu,” amesema Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesisitiza kwamba, Maafisa Utumishi wanapaswa kuwa na lugha ya staha pindi wanapowahudumia watumishi au wananchi wanaohitaji kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi mahala pa kazi.
Aidha, Prof. Shemdoe ameeleza kutoridhishwa na tabia ya Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya Morogoro anayelalamikiwa kuwajibu vibaya watumishi walioajiriwa mwaka 2025, pindi wanapomfuata kuulizia fedha zao za kujikimu lakini yeye anawaambia kama wana shida ya fedha wakakope.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kuwa mtumishi huyo yupo chini ya Mamlaka yako, namuelekeza RAS Morogoro asimamie utaratibu wa kumfungulia shauri la kinidhamu kupitia mamalaka yake ya nidhamu, ili ajibu tuhuma zinazomkabili na akitiwa hatiani aondolewe kazini na iwe fundisho kwa wengine,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, changamoto ya kukosa uadilifu ipo pia kwa watumishi wa jiji la Dar es Salaam kwani kuna Maafisa Utumishi na Maafisa wa Kanda ambao wanawahudimia vibaya watumishi wenzao, hivyo amewaasa wabadilike na iwapo watashidwa kubadilika mienendo yao hatosita kuzielekeza mamlaka za nidhamu kuchukua hatua dhidi yao na atafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yake.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi walioudhuria kikao kazi hicho, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amemuahidi Prof. Shemdoe kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa ili kujenga nidhamu bora ya utendaji kazi wa Maafisa Utumishi pamoja na watumishi wengine.
“Sisi tunayo macho na masikio na tumesikia maelekezo yako Mhe. Waziri, hivyo tunakwenda kuyatekeleza, na ninatoa wito kwa watumishi wenzangu twendeni tukafanye kazi ili tuuishi kwa vitendo kaulimbiu ya Mhe. Rais ya Kazi na Utu, tunasonga mbele,” amesema Mhe. Waryuba.
