WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupeleka huduma za upatikanaji wa vituo vya kujaza gesi (CNG) kwenye Mikoa ya Dodoma, Arusha, Morogoro na Tanga lengo likiwa kupunguza gharama za maishana kutoa huduma kwa watanzania.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo Novemba 24, 2025 jijiji Dar es Salaam kwenye kikao kazi na Menejimenti ya TPDC.
“ TPDC mmefanya kazi nzuri ya kuanzisha vituo vya ujazaji gesi kwa Jiji la Dar es Salaam lakini kuna mikoa uhitaji umekua mkubwa hivyo ni vema huduma ya vituo ikapelekwa huko pia, hivyo nielekeze Dodoma, Arusha, Tanga na Morogoro huduma hii ipelekwe.
Uhitaji wa vituo vya CNG ni mkubwa, na ni lengo la Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupunguza gharama ya maisha kwa maafisa usafirishaji, hivyo mikoa hii niliyoelekeza nayo ipelekewe huduma kwa haraka.
Aidha Mhe Ndejembi amekutana na kufanya kikao kazi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ambapo amelitaka shirika hilo kuongeza ubunifu wa utendaji wake pamoja na kuja na mikakati yenye kuleta tija kwa Taifa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ndejembi ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja na wataalamu wengine kutoka wizarani.
