HOSPITALI MPYA YA RUFAA LINDI KUANZA KUTUMIKA– DKT. SAMIZI


Serikali imesema majengo mapya ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Lindi yataanza kutumika hivi karibuni, hali itakayopunguza msongamano wa wagonjwa na kuchochea utoaji wa huduma zenye tija na ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, leo Novemba 21, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya huduma za hospitali hiyo ambapo akiwa kwenye ziara hiyo, Dkt. Samizi amebaini kuwa ni majengo mawili pekee ndiyo yanayofanya kazi kwa sasa ambapo ni jengo la radiolojia CT-Scan na jengo la X-Ray huku majengo matatu yaliyosalia yakiwa bado hayajaanza kutumika.

Awali, wananchi wa mkoa wa Lindi waliishukuru Serikali kwa kuwezesha baadhi ya huduma kupatikana hospitalini hapo licha ya kuwasilisha ombi kwa Serikali wakitaka majengo hayo yaanze kutumika haraka, wakieleza kuwa hospitali ya sasa ina eneo dogo na inashindwa kuhimili idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika kupata huduma.

Dkt. Samizi amesema kuwa amepokea ombi hilo kwa umuhimu mkubwa na kuwasilisha taarifa kwa Waziri wa afya Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa kwa ajili ya hatua za mwisho za utekelezaji na maelekezo juu ya kutatua kadhia hiyo.

“Tutaendelea kuhakikisha majengo haya yanaanza kutumika mapema iwezekanavyo, salamu hizi nitazifikisha kwa Mhe. Waziri kwa ajili ya kutoa maelekezo juu ya namna gani majengo haya yatakwenda kutumika kama ambavyo azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha afya,” amesema Dkt. Samizi.

Aidha, kuanza kutumika kwa majengo hayo ya wagonjwa wa nje (OPD) jengo la dharura (EMD) na radiolojia yanatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kibingwa, kupunguza msongamano na kuimarisha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi wa Lindi

Post a Comment

Previous Post Next Post