HAKIKISHENI MRADI WA NJIA ZA KUSAFIRISHA UMEME ZINAKAMILIKA KWA WAKATI MHE. NDEJEMBI


Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkandarasi  anayetekeleza mradi wa njia za kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma kuhakikisha  kuwa kazi za njia za  kusafirisha umeme zinakamilika kwa wakati uliopangwa.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Novemba 27,2025 Mkoani Pwani wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua njia za kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma  ikiwa ni baada ya kukamilika kwa mradi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere(JNHPP).

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika kutekeleza mradi huu na imedhamiria kuboresha miundombinu ya umeme nchini ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi na sekta za uzalishaji, hivyo tuhakikishe hadi Juni 2026 mradi huu uwe umekamilika”. Amesisitiza Mhe.Ndejembi.

Aidha Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa ubora wa kazi lazima uzingatiwe ili miundombinu iweze kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi kwa ufanisi ili wananchi wapate umeme wa kutosha huku akiwataka TANESCO kuweka maridhiano na wakandasi hao pamoja na kuhakikisha rasilimali zote muhimu zinapatikana kwa wakati ili  utekelezaji wa mradi huo uendelee kwa uharaka zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Bw. Lazaro Twange ameeleza kuwa Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania imewekeza fedha zaidi ya Trilioni 13.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo 5 vya kupokea na kupooza umeme pamoja na vituo 35 vya njia za kusafirisha umeme.

“Baada ya kukamilika kwa Bwawa la kufua umeme la JNHPP tunaendelea na ujenzi wa vituo na njia za kusafirishia umeme kutoka JNHPP Mpaka Chalinze ambapo kuna kituo cha kupokea na kupoza umeme na badae kuusafirisha mpaka kituo cha Zuzu Dodoma ambacho kitaharakisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Dodoma ,Singida, Tabora na Mikoa mingine ya jirani.”Ameeleza Bw. Twange

Katika Ziara hiyo Mhe. Waziri Ndejembi aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kyobya, Mkuu wa Wilaya ya Chalinze, Wataalamu kutoka TANESCO pamoja na Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati.

Post a Comment

Previous Post Next Post