DKT.KIJAJI: UKARABATI WA HOTELI MIKUMI KUINUA UTALII


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amefanya ukaguzi wa ukarabati mkubwa unaoendelea katika Hoteli ya Mikumi iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, hatua inayotarajiwa kuinua kiwango cha huduma za utalii na kuongeza ushindani wa hifadhi hiyo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hoteli hiyo, inayomilikiwa na mwekezaji Gullam Abbasi, inafanyiwa ukarabati wa kisasa utakaoiwezesha kutoa huduma za kimataifa na kuongeza uwezo wa kupokea wageni ndani ya hifadhi. 

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya kazi hiyo leo Novemba 25, 2025,  Mhe. Dkt. Kijaji amesema ukarabati huo unaojumuisha uboreshaji wa vyumba, maeneo ya burudani na huduma nyingine muhimu kwa watalii ni uthibitisho wa ushirikiano imara kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya utalii.

“Uwekezaji huu ni mfano wa namna sekta binafsi na Serikali zinavyoweza kushirikiana kuleta mageuzi makubwa. Hoteli hii ikikamilika itaongeza viwango vya huduma, kuvutia wageni wengi na kuongeza mapato ya nchi. Nawaomba wawekezaji wengine wajifunze kutoka kwa mfano huu wa  Abbasi,” amesema.

Aidha, amempongeza mwekezaji huyo kwa kuamua kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi, hatua inayosaidia kuimarisha uhifadhi pamoja na kuongeza ajira na fursa za kiuchumi kwa wananchi.


“Natoa pongezi za dhati kwa Bwana Abbasi kwa kuwekeza ndani ya hifadhi. Huu ni uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa uhifadhi, kwa jamii na kwa uchumi wa Taifa. Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wawekezaji wanaochangia kukuza sekta hii muhimu,” amesema Waziri Kijaji.


Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo wa malazi ndani ya hifadhi zake kwa kushirikiana na wawekezaji binafsi,  unaolenga kuongeza idadi ya vyumba, kuboresha viwango vya huduma na kuendana na ongezeko la watalii linaloongezeka mwaka hadi mwaka ambapo baada ya kukamilika, Hoteli ya Mikumi inatarajiwa kuwa ya kwanza ndani ya hifadhi hiyo kutoa huduma za kiwango cha kimataifa ikiwa na vyumba 46 vya kulala wageni, bwawa la kuogelea, ukumbi wa mazoezi , sauna, eneo la kuota moto, pamoja na sehemu maalum kwa watoto.


Miundombinu hiyo inatarajiwa kuongeza idadi ya wageni na muda wanaokaa hifadhini, hatua itakayoongeza mapato ya uhifadhi  hasa ikizingatiwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imeendelea kuwa kivutio maarufu kwa watalii wa ndani kutokana na urahisi wa kufikika, gharama nafuu na mazingira rafiki kwa familia na ni hifadhi pekee nchini inayomwezesha Mtanzania kuingia akiwa na gari lake binafsi.

Post a Comment

Previous Post Next Post