DKT. MWIGULU: TUTAILINDA TANZANIA NA RASILIMALI ZAKE KWA GHARAMA YOYOTE


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na Wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Novemba 25, 2025, ambapo amesisitiza dhamira ya Serikali kulinda maslahi ya taifa na rasilimali zake kwa gharama yoyote.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa Watanzania kuwa makini na makundi ya watu wanaotaka kuichafua nchi na kuhatarisha amani na maslahi ya taifa. Amesema Tanzania ni taifa lenye neema na rasilimali nyingi, jambo linalovutia watu wasiolitakia mema taifa hilo.

> “Kuna watu hawatupendi. Wanamezea mate rasilimali zetu. Tanzania sio masikini, ndiyo maana wengine wanatamani mabaya yajitokeze ili waweze kunufaika. Ninasisitiza: tutailinda Tanzania na rasilimali zake kwa gharama yoyote ile,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kutanguliza uzalendo, kulinda amani na kuzuia kutumiwa kufanya vitendo vinavyoweza kuiharibu nchi.


> “Kila mmoja abebe hili kwa uzito. Tumuombe Mungu na tuilinde Tanzania. Viongozi katika ngazi zote mnapaswa kuwa makini na kila anayeingia katika maeneo yenu,” amesema.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi, akibainisha kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa ya sheria yanayompa nguvu mkandarasi Mtanzania kushindania miradi mikubwa.


> “Hatutaushinda umasikini tukiamini sekta binafsi ni adui. Rais Samia amebadilisha sheria ili mkandarasi Mtanzania apewe nafasi kubwa, na wakandarasi wakubwa waombe sub-contract kwake. Hii itafungua fursa nyingi kwa vijana wetu,” amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post