Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa barabara ya Ruvu-Milo yenye urefu wa Kilomita 11 iliyojengwa kwa kiwango cha changarawe.
Akiongea kwa niaba ya wananchi hao, Mwenyekiti wa kijiji cha Kitonga, Bw. Mohamed Mtulia ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kutekeleza mradi huo ambao umeondoa vikwazo katika barabara hiyo kwani sasa wananchi wanazifikia huduma mbalimbali za kijamii kwa urahisi.
Kwaupande wake, Bw. Yohana Underson mkazi wa kijiji cha Milo ameipongeza TARURA kwa kutekeleza mradi huo na kwamba hapo awali changamoto ya barabara hiyo ilikuwa kubwa hasa kipindi cha masika.
Akielezea juu ya utekelezaji wa mradi huo, Msimamizi wa mradi kutoka TARURA wilaya ya Bagamoyo, Mhandisi Benard Mwita amesema kwa upande wa eneo la Ruvu tayari wamekamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 11 uliohusisha pia kuinua tuta la barabara na kujenga boksi kalavati tatu.
Ameeleza kuwa mradi huo umewanufaisha wananchi hususani katika vijiji vya Kitonga, Milo na Migude.
"Awali eneo hili lilikuwa halipitiki kutokana na kujaa maji lakini kwa ujio wa mradi huu sasa barabara inapitika na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na Kijamii", amesema Mhandisi Mwita.
Ujenzi wa barabara hiyo umetekelezwa kupitia mradi wa RISE programu ya uondoaji vikwazo katika barabara (Bottleneck) kwa mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.