Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameendeleza kampeni zake katika Kata ya Ihumwa kwa kueleza mikakati ya kuboresha sekta ya elimu na kuinua uchumi wa wananchi kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kijamii na biashara.
Katika mikakati yake ya kuboresha elimu, Mavunde amepanga kutoa kompyuta mpakato (laptop) kwa shule zote za msingi na sekondari katika jimbo hilo, kwa ajili ya shughuli za kuchapisha mitihani na matumizi ya walimu wakuu. Mpango huo unatarajiwa kukamilika kufikia mwezi Januari, na unatajwa kuwa ni wa kipekee katika historia ya elimu nchini.
"Kila Mwalimu Mkuu na Mkuu wa shule ofisini kwake atakuwa na kompyuta mpakato kwa shule zote za jimbo la Mtumba, pamoja na Kompyuta na mashine za kudurufu mitihani zile gharama za mtihani mnazotoa wazazi nitazibeba mimi mbunge wenu" amesema Mavunde
Kwa upande wa Mtaa wa Chang’ombe, Mavunde amesema kuwa Shule ya Msingi Jenerali Msuguri, ambayo ni miongoni mwa shule kongwe katika eneo hilo, itafanyiwa ukarabati mkubwa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na Serikali tayari imetenga shilingi milioni 340 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa, majengo ya utawala na vyoo.
Ili kuunga mkono juhudi hizo, Mavunde ameahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji na tofali 2,000 kusaidia utekelezaji wa kazi hiyo huku akieleza mpango wa kujenga uzio wa shule hiyo kwa ajili ya kulinda usalama wa wanafunzi kutokana na shule hiyo kupakana na barabara kuu.
Katika sekta ya biashara, amepanga kujenga soko kubwa la mboga mboga katika eneo la Chang’ombe ili kuifanya Ihumwa kuwa kituo kikuu cha biashara ya mazao ya mboga mboga, hatua hiyo inayolenga kuwaondolea wakulima na wafanyabiashara wa eneo hilo adha ya kusafirisha bidhaa zao hadi mjini.
Vilevile, Mavunde amepanga kuchimba kisima cha maji kwa ajili ya wakulima wa mboga mboga ili kuwawezesha kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji katika kilimo cha umwagiliaji.
Mpango huo kwa ujumla unalenga kuboresha huduma za kijamii, kuongeza kipato cha wananchi na kuifanya Ihumwa kuwa kitovu cha maendeleo katika Jimbo la Mtumba.
Tags
Siasa
