Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Peter Mavunde, ameahidi suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji katika Jimbo la Mtumba, Kata ya Mtumba, akieleza kuwa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imetenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima 18 katika eneo la Nzuguni A, kati ya hivyo visima vitatu vimekwishakamilika.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtumba, Mavunde amesema kuwa ndani ya muda mfupi wananchi wa Mtumba watasahau kabisa kero ya maji, kwani serikali ya awamu ya sita ina dhamira ya kweli ya kuboresha huduma za jamii vijijini na mijini.
“Tatizo la maji Mtumba linaisha! Rais wetu mama Samia ametoa fedha za kuchimba visima 18, vitatu vimekwishakamilika, na muda si mrefu maji yatapatikana kila mtaa,” alisema Mavunde
Mbali na changamoto ya maji, Mavunde amegusia pia tatizo la kivuko katika Mtaa wa Mtumba, akieleza kuwa Mh. Rais amekuwa akiweka utaratibu wa kutoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo, amesema fedha zikishatoka, wananchi wa Mtumba watanufaika kwani tayari wapo wawekezaji maarufu walioonesha nia ya kuwekeza na kujenga miundombinu katika eneo hilo.
Kuhusu changamoto ya eneo la makaburi, Mavunde amesema amelipokea kwa uzito na ameahidi kulifanyia kazi mara tu atakapopata ridhaa ya wananchi kuwa mbunge wa Mtumba.
Aidha, Mavunde ameahidi kuanza ujenzi wa shule ya msingi katika Mtaa wa Majengo ili watoto wasitembee umbali mrefu kufuata elimu, sambamba na kukamilisha ujenzi wa sekondari ya Vikonje A ili kupunguza mwendo wa wanafunzi wanaosafiri kila siku, huku akiahidi pia kufuatilia na kuhakikisha jengo la mama na mtoto linakamilika kwa wakati ili kuboresha huduma za afya kwa akina mama na watoto.
Mavunde amesema hajaadithiwa matatizo ya wananchi, bali anayajua mwenyewe, kwa kuwa amepita mtaa kwa mtaa, hivyo changamoto hizo zimekaa moyoni mwake, na ndizo zinazompa nguvu ya kugombea ili aweze kuzitatua kwa vitendo
