Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, leo amehitimisha kampeni zake katika kata ya Chihanga na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Akizungumza katika mkutano huo wa kuhitimisha kampeni, Mavunde amesema yupo tayari kutumikia wananchi wa Jimbo la Mtumba kwa uaminifu na kujituma endapo watampa ridhaa ya kuwa Mbunge wao.
Mavunde ameahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo ikiwemo miundombinu ya elimu, afya, maji, umeme, barabara, masoko, sekta ya michezo na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Amesema dhamira yake ni kuona maendeleo yanawafikia wananchi wa mitaa yote na kuhakikisha huduma muhimu zinaboreshwa kwa manufaa ya wote.
Katika sekta ya elimu, Mavunde ameahidi kwamba kwa kata ambazo shule zipo umbali mrefu, atahakikisha ujenzi wa shule mpya unaanzishwa ili kupunguza adha kwa wanafunzi. Aidha, amesema atahakikisha walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wanapatiwa kompyuta mpakato kwa ajili ya kurahisisha kazi zao za kitaaluma, na kununua mitambo ya kudurufu mitihani ili kusaidia wazazi kuepukana na gharama.
Kwa upande wa afya, Mavunde amesema atahakikisha zahanati zinazostahili kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya zinaboreshwa ipasavyo, sambamba na kuboresha majengo ya huduma za mama na mtoto. Ameongeza kuwa ataendeleza kliniki za madaktari bingwa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kufungua Antony Mavunde Foundation itakayojikita katika kusaidia wazee na watoto wasiojiweza katika jimbo hilo.
Kuhusu upatikanaji wa maji, Mavunde amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa ambapo visima vitatu vimekwishachimbwa kati ya 18 vilivyopangwa kuchimbwa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, hatua ambayo inalenga kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Akizungumzia sekta ya umeme na barabara, Mavunde amesema Serikali tayari imeanza kutekeleza mradi wa umeme tangu mwezi Julai mwaka huu, na baadhi ya maeneo tayari yamefikiwa na miundombinu hiyo huku maeneo yaliyosalia yakitarajiwa kufikiwa hivi karibuni. Kuhusu barabara, ameahidi kununua greda la jimbo litakalotumika kufungua, kusafisha na kukarabati barabara zote, kujenga vivuko pamoja na makaravati ili kurahisisha usafiri na mawasiliano ya wananchi.
Aidha, katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Mavunde ameahidi kuhakikisha kila kata inakuwa na soko la kujitegemea, kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo, na kutoa elimu ya fedha ili kuwaepusha wananchi na mikopo isiyo rafiki (mikopo chechefu). Pia ameahidi kuwawezesha vijana wa bodaboda kumiliki vyombo vyao vya usafiri. Kuhusu michezo, Mavunde ameahidi kujenga kituo cha michezo Ipala na kuendeleza mashindano ya Mavunde CUP ili kuinua vipaji na kukuza michezo katika Jimbo la Mtumba.
