UJENZI WA DARAJA LA MAWE KUONDOA KERO YA MAFURIKO MANISPAA YA MPANDA


Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha kwa asilimia 100 ujenzi wa daraja la Mawe la Kigamboni Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi, ukilenga kuondoa kero ya muda mrefu ya wananchi kushindwa kuvuka kwa sababu ya mafuriko ya maji hususani wakati wa masika.

Hayo yamesemwa na Fundi Sanifu kutoka TARURA, Wilaya ya Mpanda Bw. Paschal Sindani wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Mwaka 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi na kuongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umegharimu Shilingi Milioni 296 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa RISE.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha mawasiliano na usafiri kwani kabla ya hapo wananchi walikuwa hawawezi kuvuka kwenda upande wa pili  wa mto, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo utasaidia wakazi wa Kata tatu za Makanyagio, Shanwe na Misukumilo.

Bw. Sindani ameongeza kuwa mradi huo umehusisha ujenzi wa daraja la mawe lenye midomo mitatu ya kupitisha maji, ujenzi wa mabawa ya daraja, tuta kubwa la daraja na ufunguzi wa barabara mita 450.

Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi, amesema hapo awali wananchi walikuwa wakipata changamoto ya kushindwa kuvuka hasa wakati wa mvua kunyesha lakini leo limekuwa jambo la faraja, heshima na la kujivunia kwani sasa wananchi watavuka bila tatizo lolote.

Ussi amesisitiza wananchi kuendelea kuuthamini  ujenzi wa barabara hiyo kwa kuona wanaowajibu wa kuulinda ili uweze kudumu kwa muda mrefu.

Hawa Kizito, ambaye ni mkazi wa mtaa wa Shanwe ameishukuru serikali kwa daraja hilo kwani utakwenda kuokoa maisha ya wanafunzi wengi na wanawake wajawazito ambao walishindwa kuvuka na wakati mwingine walipojaribu kuvuka walipoteza maisha kwa kusombwa na maji.

Post a Comment

Previous Post Next Post