MONGELLA AZINDUA KAMPENI ZA NDEJEMBI JIMBO LA CHAMWINO


MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, Deogratius Ndejembi ameahidi kukamilisha ujenzi wa daraja  la Nzali lenye thamani ya Shilingi bilioni 14.5, ambalo linalenga kumaliza changamoto ya usafiri inayowakumba wakazi wa tarafa Itiso na Chilonwa za jimbo hilo hususan nyakati za mvua.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 08, 2025 katika Kijiji cha Nzali kilichopo Kata ya Chilonwa, Ndejembi amesema tayari ameshaanzisha mradi huo wakati wa muhula wake uliopita na sasa anahitaji kupewa nafasi nyingine ili kuukamilisha kwa maslahi ya wananchi. 

Amesema kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa maeneo hayo na litarahisisha usafirishaji wa mazao, huduma za afya na elimu.

“Wananchi wangu walikuwa wanakabiliwa na adha kubwa kila mvua inaponyesha. Lengo langu ni kuhakikisha daraja hili linakamilika kwa wakati ili kuunganisha kwa urahisi tarafa zote,” alisema Ndejembi. 

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa kama hiyo ni sehemu ya dhamira ya kweli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa CCM, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Chamwino.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Mongela ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kuamka mapema na kwenda kupiga kura, siku ya tarehe 29 Oktoba.

Post a Comment

Previous Post Next Post