MADEREVA WA SERIKALI WAPEWE MAFUNZO KUENDANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA: MAJALIWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maelekezo kwa waajiri na wasimamizi wa Madereva wa Serikali nchini kuhakikisha wanawapatia mafunzo ya mara kwa mara madereva hao ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia yatakoyowasaidia kumudu magari ya kisasa yanayotumia teknolojia mpya.

Maelekezo hayo ameyatoa leo tarehe 02 Septemba, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la Nne la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST) linaloongozwa na kauli mbiu 

“Dereva wa Serikali, Epuka ajali, Linda gari lako na watumiaji wengine wa barabara na Mwezi Oktoba Shiriki Uchaguzi Mkuu”.

“ Mabadiliko hayo ya teknolojia yazingatie mitambo mnayotumia, vifaa vya kisasa na mabadiliko ya mashine za kisasa ambazo TEMESA watasaidia juu ya jambo hilo, hivyo mafunzo haya ni muhimu", amesema Majaliwa.

Ameelekeza pia Waajiri kuhakikisha wanaweka mpango mzuri wa utengenezaji wa magari sambamba na upangaji wa ratiba za kila siku ikiwemo kupatiwa muda wa kupumzika kwa Madereva hao ili kuwezesha kutekeleza majukumu yao vizuri na kwa ufanisi.

Aidha, Amewataka Madereva wa Serikali kufanya kazi kwa nidhamu na weledi katika utendaji wa majukumu yao ikiwemo kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali pamoja na kuwa nadhifu wakati wote.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameeleza kuwa Kongamano hilo litajadili changamoto mbalimbali ambazo Madereva wanakabiliana nazo, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano wa Chama hicho  ambapo maazimio ya kongamano hilo yatakuwa chachu ya maboresho ya taaluma hiyo ikiwemo mafunzo, ajira kwa usawa wa kijinsia na matumizi salama ya magari ya kisasa.

Amefafanua kuwa Madereva wa Serikali ni mhimili muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali kwani ndio wanaohakikisha usafiri wa Viongozi na Watumishi unakuwa Salama, wenye ufanisi na unaoendana na hadhi ya Taifa la Tanzania.

Ulega ametoa wito kwa Madereva wa Serikali kuendelea kuwa na nidhamu, uadilifu na uzalendo ambao ndio msingi wa heshima ya kada hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika masuala yote yanayohusu kada hiyo.

Naye, Katibu wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), Castro Nyabange amemuomba Waziri Mkuu kuwasisitiza waajiri kutenga bajeti mahsusi za mafunzo kwa madereva ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za matengenezo ya magari ya Serikali.

Chama cha Madereva wa Serikali kimeanzishwa tangu mwaka 2013 na kusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndan mwaka 2015  kwa Na. ya Usajili S. A 20314 ambapo hadi sasa kina jumla ya wanachama 8,387.

Post a Comment

Previous Post Next Post