Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu leo Septemba 14, 2025 Songea Mjini Mkoani Ruvuma ameshiriki ufunguzi wa Kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro, akiwaomba maelfu ya wananchi waliohudhuria Uzinduzi wa kampeni hizo kumchagua Dkt. Ndumbaro na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika hotuba yake, Kingu amemtaja Dkt. Samia kama Kiongozi mwenye kudhamiria kuwatumikia wananchi wake muda wote, akimshukuru kwa hatua kubwa za maendeleo zilizopigwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa serikali ya awamu ya sita suala ambalo limewezesha ustawi na ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.
Ameitaja miradi ya afya, elimu, upatikanaji wa maji safi na salama, Usambazaji wa umeme kwenye Vijiji na Mitaa yote nchini pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji nchini kama sehemu ya mambo yaliyotekelezwa kwa kiasi kikubwa, akisema hilo ndilo linalowapa sababu za kuendelea kumnadi Dkt. Samia Suluhu Hassan wakitamani aendelee kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Tags
Siasa
