Hakamatiki, ndio msamiati sahihi unaoweza kutumika kuakisi utofauti wa kishindo cha mikutano ya kampeni za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, ukilinganisha na vyama vingine vilivyozindua kampeni.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, tathmini ya siku tano tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi zitakazodumu kwa siku 60, inaonyesha Dkt Samia amepata uungwaji mkono kutoka kwa wananchi, tofauti na washindani wake.
Wachambuzi hao, wamekwenda mbali zaidi na kusisitiza, katika mikutano yote 10 ya kampeni za mgombea huyo, imefurika maelfu ya wananchi waliokwenda kusikiliza ahadi zake.
Ukiacha maelfu ya wananchi wanaofurika katika mikutano hiyo, wachambuzi hao, wamesema ni mgombea huyo wa CCM pekee, ndiye aliyefanya mikutano mingi na mikubwa ya kampeni, kuliko mshindani wake yeyote.
Katika siku hizo tangu kuanza kwa kampeni ukiacha CCM, vyama vingine vilivyozindua kampeni ni Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Wakulima (AAFP), UDP na Chama cha Kijamii (CCK), huku vingine vikitamba kufanya uzinduzi wa kampeni siku chache zijazo.
Kati ya vyama vyote vilivyozindua kampeni hizo, Dkt Samia amefanya mikutano 10 huku mgombea mwenza wake, Dkt Emmanuel Nchimbi akiendelea kuchanja mbuga Kanda ya Ziwa.
Ukiacha CCM, CUF imefanya mkutano mmoja wa kampeni za urais, kama ilivyo kwa CCK na Chaumma, huku AAFP ikifanya miwili mkoani Morogoro.
*Hakamatiki*
Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Siasa na Jamii, Philemon Mtoi amesema ndani ya siku tano tangu kuanza kwa kampeni ni Dkt Samia ndiye aliyeonekana kuvutia wananchi wengi zaidi ukilinganisha na wengine.
Ushahidi wa hilo, amesema unaonekana kwa namna mikutano yake ya kampeni ilivyofurika maelfu ya wananchi na inavyobebwa na shamrashamra.
“Siku tano hizi kama ukifanya tathmini ni kweli Dkt Samia ameng’aa ukilinganisha na wagombea wengine, hata ukisema anabeba watu, beba na wewe tuone kama watafika idadi ile,” amesema.
Mtoi ambaye pia ni mwanazuoni wa historia katika siasa, amesema tafsiri ya siasa ni namna unavyoweza kuwashawishi watu ilimradi washawishike.
Kwa tafsiri hiyo, amesema haijalishi mgombea anatumia mbinu gani, ilimradi amefanikiwa kupata watu wengi, inatosha kuthibitisha kuwa ndiye anayeungwa mkono zaidi ya wapinzani wake.
“Kwa kiwango kikubwa mgombea wa CCM, Dkt Samia na aina ya wapinzani alionao huwezi kutarajia mtu aache kwenda kwenye mkutano wake, aende kwa wagombea wa vyama vingine,” amesema Mtoi.
Mtazamo kuwa Dkt Samia hakamatiki, umetolewa pia na mchambuzi wa siasa, Makame Ali aliyesema hilo linathibitika kwa kile kilichoshuhudiwa ndani ya siku tano za kampeni.
Ameeleza katika mikutano hiyo, kumekuwa na maelfu ya wananchi wanaohudhuria, lakini yote hayo yanatokana na uwezo wa chama husika kiuchumi na miundombinu.
“Mikutano inajaza kwa sababu wanakila sababu za kujaza mikutano yao, mojawapo ikiwa ni uwezo,” amesema.
Uthibitisho kuwa Dkt Samia hakamatiki, amesema ulianzia hata pale chama chake cha CCM kilipoitisha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kampeni, maelfu ya watu walichanga na kiasi kikubwa kilipatikana kufanikisha mchakato huo.
“Hakamatiki wala hatokamatika, hii ni sawa na mbio za riadha, kuna wengine wanajua wanaenda tu kuongeza idadi ya watu walioshiriki kwenye mbio,” amesema.
Kwa mazingira yalivyo, amesema CCM ina msingi na mfumo mzuri zaidi wa kufanya kampeni, kutokana na mtandao wake mpana, hivyo mwenye kisu kikali ndiye atakayekula nyama.
“Hakuna siasa bila fedha, ndiyo maana CCM ilitafuta watu ikachangisha na wakapata mabilioni ya fedha. Vyama vingine hata ukiitisha mkutano wa kutoa Sh milioni moja inakuwa mtihani,” amesema.
Amesema tangu mkutano wa kwanza wa Dar es Salaam, Morogoro kisha Dodoma, Dkt Samia ameshuhudiwa akijaza maelfu ya wananchi wanaokwenda kusikiliza sera zake.
Makame amesema kati ya vyama vingine vyote vya siasa, ni CCM pekee ndiyo iliyofanya mikutano mingi, hivyo ni vigumu kwa mgombea wake wa urais kukamatika.