Mgombea ubunge wa Jimbo la Kondoa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Ashatu Kijaji, leo amezindua rasmi kampeni zake katika Kata ya Pahi, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally.
Katika hotuba yake mbele ya wakazi wa kata hiyo, Dkt. Kijaji alieleza dhamira yake ya kuendeleza juhudi za maendeleo kwa wananchi wa Kondoa, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii, kuinua kipato cha wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili.
Miongoni mwa changamoto alizozibainisha ni pamoja na uvamizi wa wanyamapori, hususan tembo, kutoka Pori la Akiba la Mkungunero ambao wamekuwa wakivamia makazi ya watu na kuharibu mazao. Hivyo alimuomba dkt Bashiru kufikisha kwa viongozi wa juu wa chama changamoto hiyo kwa kupata msaada wa kuwadhibiti ilikunusuri mali na mazao ya wananchi wa eneo hilo
Kwa upande wake, Dkt. Bashiru Ally aliwahakikishia wananchi kuwa CCM imejipanga kuboresha maisha ya wakazi wa vijijini kwa kuongeza kasi ya maendeleo kupitia uanzishaji wa viwanda vidogo vinavyoongeza thamani ya mazao.
Aidha, aliwaomba wananchi wa Jimbo la Kondoa kumpigia kura Dkt. Ashatu Kijaji, akimtaja kuwa ni miongoni mwa viongozi bora wenye maono ya kuwaletea maendeleo. Aliahidi kufikisha ombi la mgombea huyo juu ya changamoto za wanyamapori kwa viongozi husika ili hatua stahiki zichukuliwe.
Uzinduzi huo wa kampeni umeashiria kuanza rasmi kwa mbio za uchaguzi katika Jimbo la Kondoa, huku CCM ikiahidi kuendeleza miradi ya maendeleo na kulinda maslahi ya wananchi.
