Waziri wa Ujenzi na mbunge aliyepita wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega, amerejesha fomu za kuwania ubunge kwa kishindo, akisindikizwa kwa maandamano ya wananchi.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Ulega alisema anaomba tena ridhaa ya kuongoza jimbo hili ili aweze kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la wana Mkuranga.
Alisema hivi sasa Mkuranga imekuwa mojawapo ya wilaya kinara kwa viwanda nchini na kwamba kazi kubwa ya awamu ijayo itakuwa ni kupeleka maendeleo kwenye jimbo hilo kwa kasi zaidi
" Kwa kazi ambayo Jemedari wetu, Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya, nina matumaini makubwa kwamba Watanzania watajitokeza kwa wingi kumpigia kura ili aendeleze pale alipoishia.
"Kwa Mkuranga wenyewe mnaona. Umeme umefika kote, shule zinajengwa, vituo vya afya vipi kila mahali na viwanda vinatoa ajira. Tujitokeze kushiriki uchaguzi ili mazuri haya yaendelee,” amesema Ulega
Wakati akienda kuchukua fomu, Ulega alitembea na msafara wake kwa takribani umbali wa kilometa tano huku kukiwa na hamasa kubwa.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umepangwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu huku kampeni rasmi zikitarajiwa kuanza kesho