UJUMBE wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii umetembelea Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele kujionea utendaji kazi wa kituo hicho kilichopo mkoani Katavi mnamo tarehe 04.07.2025.
Kituo cha Kijeshi Mlele kimekuwa kikitoa mafunzo ya kijeshi ya kati ya miezi mitatu au sita kutegemea na nafasi aliyoajiriwa nayo kwa waajiriwa wa taasisi za uhifadhi za TANAPA, TAWA, TFS na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Ujumbe huo ulioongozwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC) Fidelis Kapalata ulijionea utendaji wa kituo hicho na maendeleo ya mafunzo kwa askari wanafunzi ajira mpya za Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Katika ziara hiyo ujumbe huo ulitembelea na kukagua miundombinu ya kituo hicho ikiwamo mabweni ya wanafunzi, ofisi, uwanja wa ndege, viwanja vya mazoezi, zahanati, nyumba ya kupumzikia na nyumba za wakufunzi.
Akizungumzia utendaji kazi wa Kituo hicho, Kapalata amesema kituo hicho kimekua bora kwa kuwafundisha askari na maafisa wa jeshi hilo mbinu mbalimbali za uhifadhi kutoka katika taasisi zilizo chini ya wizara.
Amesema kila mwaka zaidi ya askari na maafisa 1,000 kutoka taasisi za uhifadhi zilizochini ya Wizara ya Maliasi na Utalii upata mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kutekeleza kikamilifu majukumu ya uhifadhi.
Kwa upande wake Afisa mwandamizi wa Uhifadhin(SCO)-Šimon Msuva amesema kwa sasa kituo kina wanafunzi 368 ambao ni ajira mpya kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ambao watapata mafunzo hayo kwa miezi sita.
"Mafunzo yanaendelea vizuri na wanafunzi wanaendelea kuiva kwa kujua mbinu mbalimbali za uhifadhi na ndani ya miezi sita watakua wameiva tayari kwenda kulinda maliasili za Taifa."
Kituo cha mafunzo cha mlele kilianza kutumika rasmi kama kiuo cha wizara mnamo mwaka 2018 baada za Wizara kupitia taasisi zake 4 za uhifadhi kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia kwenda wa kijeshi.