Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza rasmi kuijumuisha tarehe 17 Novemba katika kalenda yake ya kimataifa kama Siku ya Watoto Njiti Duniani, ikiwa ni hatua muhimu ya kutambua na kuhamasisha jitihada za kulinda maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda kamili wa ujauzito.
Hatua hii ni ushindi mkubwa kwa sekta ya afya ya uzazi duniani, na hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kupigania uboreshaji wa huduma kwa watoto wachanga, hususan wale njiti. WHO imesisitiza kuwa kuwepo kwa siku hiyo kutasaidia kuongeza uelewa, kuimarisha sera za afya na kuvutia uwekezaji zaidi katika huduma za watoto wachanga.
Tanzania imechukua nafasi ya kipekee katika mafanikio haya kupitia juhudi za muda mrefu za Doris Mollel, mwanzilishi wa Doris Mollel Foundation (DMF). Doris, ambaye alizaliwa njiti, amegeuza simulizi yake kuwa chachu ya mabadiliko kwa watoto wengine waliopitia changamoto kama alizopitia yeye.
Kwa zaidi ya miaka saba, taasisi yake imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu watoto njiti, kuchangisha na kusambaza vifaa tiba kwa hospitali nchini, na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya wanaohudumia watoto hao. Zaidi ya hospitali 20 zimepata msaada wa incubator, mashine za oksijeni, vifaa vya kupima joto, na usaidizi wa mafunzo kwa wauguzi kupitia DMF.
Akizungumzia uamuzi huo wa WHO, Doris alisema:
“Kupitishwa kwa Novemba 17 na WHO ni heshima kubwa kwa watoto njiti duniani. Kwa upande wangu binafsi na kwa Tanzania, hii ni zawadi ya juhudi za miaka mingi. Ninaamini sasa dunia itasikia kilio cha watoto hawa na kuchukua hatua madhubuti.”