Wakala wa Huduma za Misitu nchini imetakiwa kuweka mkakati wa kuzalisha miche ya kutosha kwa ajili ya kuipatia jamii sambamba na kutoa elimu ya utunzaji wa miche hiyo baada ya kupandwa lengo likiwa ni kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa ni changamoto kubwa duniani.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula, ameyasema hayo alipokuwa kwenye banda la Wakala wa Huduma za Misitu(TFS) ambao wameshiriki kama wadau muhimu wa utunzaniji wa mazingira kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani katika viwanja vya Ukumbi wa Kimataifa wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo tarehe 04.06.2025.
Katika salam zake Mhe. kitandula alisema Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wakala wa Huduma za Misitu nchini inahifadhi asilimia 32 ya ardhi ya Tanzania ambayo iko na hifadhi za misitu ya asili na kupandwa, hivyo kama wadau muhimu hatuna budi kuilinda kwa wivu mkubwa.
Mhe. Kitandula alisema uhifadhi unaofanywa na Wakala wa Huduma za misitu unaiweiwezesha nchi kuwa na vyanzo vingi vya maji vyenye uhakika lakini pia ndio umewezesha nchi kuwa na Chanzo kikubwa cha Nishati ya Umeme Cha Mwalimu Nyerere ambacho ni Cha kudumu.
“Tumekuwa tukiona mikakati mingi ya upandaji miti mkiwa na taasisi nyingine au wadau mbalimbali wa utunzaji wa mazingira jambo lisiwe kupanda miti peke yake lazima tubadili mtizamo wa kupanda miti bali tuwe na mtizamo wa kupanda kutunza na kuhakikisha inakuwa mikubwa” alisema Kitandula