TARURA YAKAMILISHA MATENGENEZO YA BARABARA YA MLOWO-MPITO-ISANSA WILAYANI MBOZI


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha matengenezo ya barabara ya Mlowo-Mpito-Isansa yenye urefu wa Km 13.4 kwa kiwango cha changarawe wilayani Mbozi mkoani Songwe. 

Barabara hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa vijiji vya Watele, Isansa, Makua na Iwezi ambavyo vinajishughulisha na kilimo cha mazao ya kahawa, mahindi na karanga ilikuwa na changamoto kubwa ya ubovu hali iliyopelekea wakazi wa vijiji hivyo kuzunguka Km 45 ili kufika katika mji wa Mlowo kwa ajili ya kulifikia soko.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Msimamizi wa mradi huo kutoka TARURA  wilaya ya Mbozi, Mhandisi Freddy Mlowe amesema kuwa barabara hiyo ilikuwa na changamoto kubwa hususani upungufu wa makavati pamoja na mifereji ya kupitishia maji ambapo kipindi cha mvua maji yalikuwa yanakatisha katikati ya barabara na kuleta uharibifu mkubwa.

"Baada ya matengenezo haya sasa imekuwa rahisi kwa wananchi kuweza kusafirisha pembejeo za kilimo pamoja na mazao yao hususani kahawa, mahindi na karanga ambayo ni mazao makuu katika wilaya yetu hii ya mbozi". 

Ameeleza kuwa matengenezo yaliyofanyika katika barabara hiyo ni pamoja na kuchonga barabara takribani Km 13, kuweka kifusi km 8, kujenga mifereji ya kupitishia maji, kujenga makalavati 'line' nane (8) pamoja na kuinua tuta katika kijiji cha Mpito.

Naye, Bw. Weekend Mahange, Mwenyekiti wa mtaa wa Shule, kata ya Mlowo ameishukuru Serikali kwa kuwatengenezea barabara hiyo kwani miaka mingi ilikuwa haipitiki hasa kipindi cha masika lakini baada ya kutengeneza mitaro barabara imekuwa inapitika katika kipindi chote cha Mwaka 

"Wananchi wa Mlowo wanategemea sana kilimo na hii ndio barabara kuu hasa kwa Kitongoji chetu hiki lakini pia majirani zetu wanaitegemea barabara hii kwa sababu  mji wa Mlowo kwa sasa umekuwa na unategemewa na watu wengi na ni soko kubwa la mazao kutoka vijijini" amesema Bw. Mahange.

Kwa upande wake, Bi Tumaini Kalinga, mkazi wa Kitongoji cha Mlowo amesema kabla ya matengenezo gharama ya kusafirisha gunia moja la mahindi kutoka kijiji cha Isansa mpaka Mji wa Mlowo ilikuwa shilingi 3000 lakini baada ya matengenezo gunia moja linasafirishwa kwa shilingi 2000 tu, ambapo kwasasa akina mama wajasiriamali wanafanya biashara zao vizuri.

Post a Comment

Previous Post Next Post