RAIA WA NCHI 71 KUINGIA TANZANIA BILA VIZA


Serikali imeingia makubaliano na nchi mbalimbali ili kurahisisha utaratibu wa viza ambapo raia wa nchi 71 hawahitaji viza wanapoingia nchini. 

kwa sasa watalii kutoka mataifa mengi zaidi duniani wanaruhusiwa kupata visa wanapowasili (visa on arrival) kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa kama Julius Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro na Zanzibar. 

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa maliasili na utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akijibu swali la Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya aliyetaka kujua ni jitihada gani zimefanyika kurahisisha upatikanaji wa VISA kwa Watalii wenye uraia tofauti wanaokuja nchini kwa mwitikio wa Tanzania the Royal Tour.

Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa utoaji wa viza nchini ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Mathalan, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha mfumo wa maombi ya viza kwa njia ya mtandao (e-Visa) unaowawezesha watalii kuomba viza popote walipo duniani bila kulazimika kufika ubalozini.

“Halikadhalika, Serikali imeboresha Kanuni za Uhamiaji za mwaka 2023 (GN 428) ambapo kwa sasa watalii wanaotumia Visitors Pass wanaruhusiwa kutembelea Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kurejea Tanzania bila hitaji la kuomba upya pasi ya kuingia nchini” Alisema Mhe. Kitandula

Suala la visa lina uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii imeimarisha ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Ndani, hususan Idara ya Uhamiaji, katika nyanja mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa takwimu za watalii na kuwa na mikakati ya pamoja ya kuvutia watalii na fursa za uwekezaji.

 Aidha, siku za hivi karibuni, Wizara kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii imetoa mafunzo ya Huduma kwa Wateja na Ukarimu kwa Maafisa wa Jeshi la Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wageni wanaoingia nchini, ikiwemo watalii

Post a Comment

Previous Post Next Post