Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo amezindua mfumo wa kidigitali wa kupokea taarifa za kero na changamoto za wananchi ambazo zitakuwa zinawasilishwa kupitia uongozi wa Mtaa.
Mfumo huo umezinduliwa sambamba na ugawaji wa simu janja(smart phones) kwa wenyeviti wa mitaa yote 222 ya Jimbo la Dodoma mjini
“Mfumo huu wa uwasilishaji wa taarifa zinazowahusu wananchi utasaidia kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa ukaribu na uharaka zaidi.
Mfumo huu utatumika kusambaza taarifa kwa haraka kwenye ofisini ya Mkuu wa Wilaya, Kwa wasaidizi wangu ofisini kwa Mbunge na kwangu mwenyewe bila hitaji la kupiga simu.
Ni mategemeo yangu kwamba simu hizi zitatumika katika kusudio lililolengwa na kusogeza huduma karibu kwa wananchi kwa kuwasilisha changamoto zao kwa wakati na kufanyiwa kazi kwa wakati”Alisema Mavunde
Mbunge Mavunde pia amekishukuru kiwanda cha kutengeneza simu kinachomilikiwa na Mtanzania kupitia Kampuni ya Raddy Electronics kilichopo Mkuranga,Pwani kwa uzalishaji wa simu hizo ambazo zitatumika kwenye mfumo huo.
Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa Dodoma Mjini Ndg. David Ndejembi amempongeza Mbunge Mavunde kwa kuwa karibu na wananchi katika utatuzi wa changamoto zao na kuahidi kuutumia mfumo huu ipasavyo kuwasilisha taarifa za wananchi kwa wakati.
Aidha Ndejembi amemshukuru Mbunge Mavunde kwa mchango wa Tsh 10,000,000 kutunisha mfuko wa SACCOS ya Wenyeviti wa Mitaa Dodoma.