DKT. KIMAMBO AFANYA ZIARA YA KWANZA MLOGANZILA, AKUTANA NA UONGOZI ATEMBELEA WAGONJWA


Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Delilah Kimambo leo amefanya ziara yake ya kwanza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mapema mwezi huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan .

Katika ziara hiyo, Dkt. Kimambo amefanya kikao na kuupongeza Uongozi wa hospitali hiyo kwa namna ambavyo unaendelea kusimamia huduma za ubingwa na ubingwa bobezi, kufanya maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma, kujituma kwa wataalam na kuchochea utoaji wa huduma bora.

Baada ya kikao hicho Dkt. Kimambo ametembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma na kukutana na wagonjwa na ndugu wa wagonjwa pamoja na kupata maoni yao kuhusu namna ambavyo wanahudumiwa hospitalini hapo.

“Nimetembelea maeneo ya kutolea huduma na kupata fursa ya kuongea na wateja wetu, wamekiri huduma ni nzuri, ni wajibu wetu kuhakikisha tunaendelea kutoa huduma bora kwa kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali ni mkubwa na lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa gharama nafuu.

Aidha, Dkt. Kimambo amesisitiza uwajibikaji, nidhamu na weledi katika kuhudumia wateja wote wanaofika hospitalini hapo kwa kuwa Watanzania wana imani kubwa na huduma zinazotolewa na watoa huduma wa hospitali hiyo.

Ikumbukwe kuwa ni mara ya kwanza kwa Dkt. Kimambo kutembelea hospitali hiyo tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Juni 16, 2025 kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Post a Comment

Previous Post Next Post