Makandarasi wazawa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuomba tenda mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya uboreshaji miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) ili kuweza kunufaika na fursa hiyo kama sehemu ya kukuza uchumi wa Tanzania na kuimarisha mzunguko wa fedha nchini.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Juni 02, 2025 Mjini Singida na Mhandisi Humphrey Kanyenye, Mratibu wa miradi ya Benki ta Diunia TARURA wakati wa utiaji saini wa miradi hiyo kwa Manispaa ya Singida, itakayohusisha ujenzi wa soko la Kimataifa la Vitunguu, ujenzi wa barabara za katikati ya Mji na Viwandani zenye urefu wa Km 7.52 pamoja na ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wa Mnung'una, utakaokuwa na urefu wa Km 2.6 na jengo la usimamizi na uratibu wa miradi hiyo.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi mzawa M/s Sihotech Engeneering Company Limited kwa kushirikiana na kampuni ya AMJ Global Mult Contractors kwa gharama ya shilingi 24, 748,966,236.05 na ukitarajiwa kukamilika mara baada ya kipindi cha miezi kumi na tano kitakachoanza Juni mwaka huu.
"Maeneo mengi tumepata wakandarasi wa Kichina lakini kwa Manispaa ya Singida tumepata bahati ya kupata mkandarasi mzawa na yeye pia amefanya kazi maeneo mengine na katika kulinganisha utendaji kazi wake kulinganisha na wakandarasi wa Kichina, Mkandarasi huyu yupo mbele kwa asilimia zaidi ya 20, “ amesema mhandisi Kanyenye.
Kulingana na mhandisi Kanyenye, kukamilika kwa mradi wa TACTIC kutaleta manufaa makubwa kwa Manispaa ya Singida ikiwemo kuongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuboresha hali ya biashara katika maeneo husika, hivyo kuchangia maendeleo ya muda mrefu ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Soko la Kimataifa la Vitunguu litajengwa mkoani Singida likitarajiwa kuwa na jengo la ghorofa mbili likiwa na eneo la kuchambua vitunguu, kukaushia vitunguu, maduka 10, Vyumba 4 vya huduma za kifedha, pamoja na maeneo mengineyo likitarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri kutoka Milioni 300 hadi Milioni 505 litakapokamilika.