Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema kutekelezwa kwa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kumekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanyonge hasa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama, ikipunguza pia asilimia kubwa ya malalamiko ya kisheria kwenye jamii sambamba na kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria.
Mhe. Sagini amebainisha hayo mapema leo Mei 05, 2025 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa kisheria Mkoa wa Kusini Pemba akisisitiza pia kwamba kampeni hiyo imeongeza pia uelewa wa wananchi kuhusu elimu ya sheria, haki na wajibu pamoja na misingi ya utawala bora sambamba na kutatua migogoro mingi kwa njia mbadala hivyo kuongeza amani, utulivu na kukuza maendeleo.
Naibu Waziri Sagini akitoa salamu za Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, mbali ya kueleza kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo umefanikiwa kutokana na ushirikiano ulipo kati ya Wizara ya Katiba na sheria na Ofisi ya Rais, Katiba, sheria, utumishi na utawala bora, akieleza kuwa ushirikiano huo umewezesha makundi maalumu ya wanawake, Watoto na wenye ulemavu kuweza kufikiwa.
"Mheshimiwa Mgeni rasmi napenda kuendelea kuahidi kwamba Wizara ya Katiba na sheria ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Hususani Waziri wake Dkt. Damas Ndumbaro na sisi wasaidizi wake tutaendelea kushirikiana na Wizara ya nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, sheria,utumishi na utawala bora pamoja na wataalamu wake katika kuhakikisha kampeni ya msaada wa kisheria inakuwa endelevu na inawafikia wananchi wote." Amesema Mhe. Sagini.
Ameeleza kuwa mashirikiano kati ya wizara hizo yamekuza zaidi ushirikiano huo ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kubadilishana uzoefu kuhusiana na urekebu wa sheria na uendeshaji wa kesi mbalimbali pamoja na kuratibu kwa pamoja majukwaa na makongamano ya ndani na nje ya nchi.
Mhe. Sagini pia amewashukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa juhudi zao katika kudumisha amani na utulivu nchini, akieleza kuwa Viongozi wao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini
Katika Hafla hiyo, Naibu Waziri Sagini aliyemuwakilisha Waziri Damas Ndumbaro, ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria (bara) Dkt. Franklin Jasson Rwezimula sambamba na Maafisa wengine kutoka Wizara ya Katiba na sheria