Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Visiwani Zanzibar Mhe. Rashid Hadid Rashid amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kubuni na kufadhili Kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, akisisitiza umuhimu wa Wanasheria wanaotekeleza kampeni hiyo kwenye Mkoa huo kuwa na mkakati madhubuti wa kuwafikia wale wote wenye uhitaji.
Mhe. Rashid amebainisha hayo leo Jumatatu Mei 05, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Kwenye Mkoani wa Kusini Pemba, katika viwanja vya Bustani ya Mwanamashungi, akieleza kuwa ni dhamira ya Rais Samia kuona haki za binadamu zinatamalaki kwenye jamii ya Kitanzania sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa usawa na haki kwa kila mwananchi.
"Mhe. Mgeni rasmi (Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mhe. Khamis Abdallah) katika masuala ya kijinsia mara nyingi wadau wengi wanaangalia wanawake na watoto lakini nataka nikuhakikishie sisi mikoani tumekuwa tukikumbana na migogoro mingi ya wanaume wakidhalilishwa na wanawake kwa baadhi ya wanawake wanaozibadilisha na kuhadaa hati za umiliki wa mali kama majengo na viwanja. Ni imani yangu kuwa kampeni hii itanufaisha jinsia zote." Amesema Mhe. Rashid huku akishangiliwa na wananchi.
Akizungumzia matarajio yake kwenye Siku tisa za utekelezaji wa kampeni hiyo kwenye Mkoa wa Kusini Pemba, ameeleza kuwa kampeni hiyo itasaidia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato kwa kutoa fursa kwa wananchi kujikita zaidi katika uzalishaji mali, kuleta utengamano wa kisiasa pamoja na kukuza utawala bora kwa wananchi na watendaji mbalimbali wa serikali kupitia elimu mbalimbali zinazotolewa.
Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kunufaika na msaada huo wa kisheria, akieleza kuwa serikali ya Mkoa huo itatoa ushirikiano wa kila hali kuhakikisha kuwa kampeni hiyo inafanikiwa katika kuakisi dhamira, maono na malengo ya Rais Samia.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa katika siku hizo tisa za utekelezaji wa kampeni hiyo ya msaada wa kisheria makundi mbalimbali yatanufaika na utatuzi wa migogoro ya ardhi, mirathi, ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa huduma za ushauri nasaha kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia.