"Dhamira ya kampeni ya Mama Samia ni kushughulikia changamoto za kisheria zinazowakumba wananchi kwa kutoa huduma za msaada wa huduma za kisheria bila ya malipo yoyote hususani kwa wanawake, watoto, wazee na wote wanaoishi katika mazingira magumu.
Ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa kila mwananchi popote alipo anaweza kupata haki yake bila kujali uwezo wake wa kifedha, rangi, dini ama jinsia yake.
Katika dunia ya sasa ambayo maendeleo ya jamii yanategemea ushiriki wa kila mtu ni lazima tuweke mazingira yatakayomuwezesha mwananchi wa kawaida kusikilizwa, kuzijua haki zake na kupata msaada pale anapodhulumiwa au kuingia kwenye matatizo ya kisheria.
Bila ya shaka utekelezaji wa kampeni hii utaleta muamko mkubwa kwa watanzania wa kufahamu haki zao na namna ya kuzifuatilia hasa kwa wale wanaoishi maeneo ya mbali na wenye uwezo mdogo kama nilivyosema.
Kwakuwa kampeni hii inatekelezwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa wito kwa Viongozi na watendaji wa Wizara zetu mbili zinazoshughulikia masuala ya sheria, kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa kampeni hii katika kutafuta rasilimali fedha na nyenzo nyingine zinazohitajika pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu.
Nimefurahi kuona kwamba wapo hapa viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushirikiano wa karibu unaofanywa na wizara zetu hizi mbili ni mfano wa kuigwa katika kuendeleza, kuulinda na kuudumisha muungano wetu ambao mwaka huu umetimiza miaka 61 ukiwa na mafanikio makubwa.
Ndugu wananchi, naipongeza kaulimbiu ya kampeni hii inayosema msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo. Ni dhahiri kuwa kaulimbiu hii inaenda sambamba na misingi ya Katiba zetu pamoja na mipango ya serikali katika kusimamia na kuendeleza misingi ya haki na usawa."- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa kisheria Mkoa wa Kusini Unguja leo Mei 10, 2025.